July 7 2010
Mungu ametubariki sana watanzania na waafrika kwa ujumla. Unaona jinsi jua linavyotoka kwa muda muafaka na kuzama kwa muda muafaka. Summer hii nipo Ujerumani kwenye mji ujilikanao kama Wolfenbüttel. Watu ni wema na wanapenda sana watanzania na nchi yetu ya Tanzania. Kila mwaka tunakuwa na Misa ijulikanayo kama "Afrikanische Messe". Kwenye hii Misa tunaimba nyimbo za Kiswahili na lugha nyingine za Kiafrika. Mwisho wa Misa watu ukaa pamoja na kuwa na mlo wa pamoja wa mchana. Tunawaeleza sana mambo ya kwetu nao wanafurahi sanas.
Lakini huku sasa hivi jua linazama saa 4 na kitu usiku. Yaani kwangu inakuwa shida sana kusinzia. Kwani najisikia kama kulala saa 12 na nusu jioni nikiwa nyumbani (Tanzania), lakini saa inaonyesha saa 5 usiku. Maajabu hayo. Tena nasikia kaskazini zaidi huko basi kwa sasa ni mchana tu masaa yote. Nimeshuhudia hilo nikuwa kwenye ndege nikisafiri kutoka Nice (Ufaransa) kwenda Hannover (Ujerumani) saa 6 usiku, niliona mwanga wa jua huko maeneo ya Kaskazini mwa dunia yetu. Nadhani ingekuwa Tanzania watoto wangecheza mpira wa miguu usiku kucha na wazazi wasingelalamika kwa sababu hakuna giza. Basi wangeenda shule wakiwa wamechoka. Ng'ombe, mbuzi, Kuku na wanyama wengine wangekula masaa 24. Kwa wale waliosoma Rubya Seminari miaka ya nyuma, basi tungepiga "msipaka" (Kupiga msipaka ni kusoma usiku wakati wengine wamelala) bila gharama ya mafuta ya taa. Lakini je, asubuhi mtu angeamkaje? Wavuvi wa dagaa wangepata hali ngumu kama mwezi tu unawasumbua. Kwenye meli ya Victoria au Serengeti, daraja la kwanza na la pili kulala wangekosa wateja kabisa. Tukumbuke kuwa wakati wa majira ya baridi huko ni giza masaa mengi au hata yote! Sijui hali yetu ingekuwaje! Basi tufurahie mazingira yetu na tuyaboreshe ili tuishi kwa furaha na hali bora zaidi. Mungu ametupa uwezo wa kuboresha mazingira yetu, sema tu mara nyingine hatutumii kabisa uwezo huo.
Kutokana na hali hiyo ninayoipata sasa nitaandika juu ya mtazamo tofauti wa muda wa watu mbalimbali duniani. Tofauti hii inatokana na tofauti ya mazingira, utamaduni na shughuli za kila siku. Mkulima atakuwa na mtazamo tofauti wa muda na mvuvi au mwindaji. Mkulima shughuli zake ni mchana na mvuvi mara nyingi ni usiku (Nazungumzia hasa wavuvi wa mkoa wa Kagera katika ziwa Victoria nilio na uzoefu nao).
Naomba mchango wa mawazo yenu juu ya muda (Time Concept) ili niweze kufanikisha mpango huo nilio nao. Nitaanza na mada ifuatayo kwa Kiingereza "Liturgical Year and Bahaya Concept of Time". Kichwa hiki sijakiweka vizuri lakini ndiyo nia yangu ya kuandika juu ya Muda katika mila za Wahaya wa kale na wa sasa. Nitajaribu kuoanisha na mtazamo wa Mwaka wa Kanisa (Latin Rite). Ninajaribu kutafiti ni jinsi gani tunaweza kuoanisha Ukristu wetu na Utamaduni wetu ulio mzuri hasa katika mzunguko mzima wa mwaka.
Tunaweza kujiuliza swali, Kwa nini kila mwaka hasa Desemba karibu na Krismasi au Noeli, huwa inakuwa vigumu kupata tiketi ya kusafiri kwenda mikoani? Je, watu wanaosafiri kipindi hicho wanaenda tu kusherekea Krismasi nyumbani au kuna mambo mengine ambayo yameunganishwa kwa nia nzuri na siku hiyo? Kama huamini jaribu kwenda Stendi ya mabasi ya mikoani Ubungo mwisho wa mwaka, ulizia tiketi ya Bukoba, Mwanza, Moshi au Arusha na utanipa jibu. Nadhani kwa mtazamo wangu, ambao bado naufanyia utafiti zaidi, kuna jambo zuri tu la kimila ambalo limeunganishwa na sherehe ya Krismasi na mwisho wa Mwaka.
Nami kwa upande wangu natamani sana kufanya sana utafiki juu ya mtazamo wetu wa muda kwa ujumla na kuhusu mambo ya imani yetu. Karibuni katika mjadala huu kwa kutoa mawazo, habari muhimu, taarifa, hadithi na maswali juu ya mada hii.
G. Mutarubukwa
27062008101
by ijue-liturjia-takatifu.over-blog.com