Overblog
Edit post Follow this blog Administration + Create my blog
liturjia-takatifu.over-blog.com's name

Hii blog ni kwa ajili ya kuitikia mwaliko wa Mtaguso wa pili wa Vatikano wa kuwafanya wakatoliki wote waifahamu liturjia takatifu wanayoiadhimisha. Nitatoa utafiti wangu juu ya liturjia na nitakuwa tayari kujibu maswali yenu juu ya liturjia. Karibuni sana!The aim of this blog is to impart liturgical knowledge to the people of God. It targets mainly the people from the swahili speaking countries. Welcome for the sharing of knowledge about our liturgy!

Liturjia ni nini?

Liturjia  na Elimu katika Liturjia ni nini?

Leo nina mambo mawili ya kuzungumzia na kushirikishana kwa ufupi tu. Kwanza ni kueleza undani wa Liturjia na pili kueleza kile mtu anachofanya anapojifunza kuhusu liturjia. Nilikuwa siku moja natembea natembea hapo CUEA (The Catholic University of Eastern Africa) huko Nairobi, mtu mmoja akatambulishwa kwangu na kuambiwa kuwa nafundisha Liturjia. Basi swali alilotoa la kwanza ni: “Liturjia ni nini?” Akaongeza kusema kuwa aliposoma seminari miaka ya nyuma alifundishwa kuhusu mambo yale ambayo siyo liturjia tu na ndiyo anayokumbuka tu. Kwa hiyo mimi sitazungumzia hayo mambo ambayo siyo liturjia ili nisiwaweke katika kishawishi cha kukumbuka hayo tu. Nitaeleza kwa kifupi liturjia na masomo ya liturjia kama sehemu muhimu ya Teolojia.

Liturjia ni nini?

Palm-Sunday-Mass-Vatican--NW7SyOwC3Rl.jpg

Liturjia ni adhimisho la Kanisa la Fumbo la Kristu, yaani Fumbo la Pasaka (Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristu)(rejea Sacrosanctum Concilium 5, 6, 7). Liturjia ni tendo takatifu la Kristu (Kichwa) na Kanisa lake (Mwili wa Kristu) linaloonyesha na kuwaletea watu Ukombozi uliokamilika katika Kristu ili tuweze tena kuwa na mahusiano mazuri au mwungano na Mungu na Kanisa lake lote kwa ajili ya kuwakomboa na kuwatakatifuza watu wa nyakati zote. Katika liturjia tendo la Ukombozi la Kristu linatufikia sisi leo hii na muda ule ule tunapoadhimisha liturjia. Kwa njia ya liturjia, tendo hilo la Ukombozi litavifikia vizazi vijavyo mpaka Kristu atakavyokuja tena mara ya pili. Ndiyo maana katika Misa wakati wa Sala ya Ekaristi baada ya mageuzo tunatangaza fumbo hilo la imani tukisema “Ee Bwana tunatangaza kifo na kutukuza ufufuko wako mpaka utakapokuja”.

Liturjia ni chemichemi ya Ukombozi wetu. Liturjia ni mlango unaotufungulia mafumbo makuu ya wokovu wetu na kutuingiza katika umoja mtakatifu na Mwenyezi Mungu. Ndiyo maana Fr. John Zuhlsdorf ameandika juu ya kuokoa liturjia ili kuokoa ulimwengu, kwa kiingereza “ Save the Liturgy, save the world”.  Ndiyo maana Mtaguso wa pili wa Vatikano umeielezea liturjia kama chemchemi na kilele cha shughuli zote za Kanisa (Sacrosanctum Concilium 10). Ni katika liturjia Kristu anaendeleza, katika Kanisa na kwa njia ya Kanisa, kazi ya Ukombozi wa watu.

Papa Pius XII katika barua yake iitwayo Mediator Dei ya mwaka 1947, alieleza kuwa Liturjia ni tendo la ibada ambalo Mkombozi wetu kama kichwa cha Kanisa anamtolea Mungu Baba, na pia ni tendo la ibada ambalo jamii ya waamini inamtolea Kristu, na kwa njia ya Kristu (yaani kupitia Kristu kama tunavyosali kila tunapomaliza sala, kwa njia ya Kristu Bwana wetu, Amina) inamtolea Mungu Baba. Kwa kifupi liturjia ni tendo linalotolewa na Kanisa zima, Mwili wa Kristu, la kumwabudu, kumtukuza, kumshukuru na kumwomba Mwenyezi Mungu. Mawazo haya ndiyo tunayakuta katika maelezo ya liturjia ya Mtaguso wa pili wa Vatikano (Sacrosanctum Concilium 7).

Liturjia ni adhimisho la Fumbo la Pasaka katika Ibada ya Misa Takatifu (Ekaristi), maadhimisho ya Sakramenti mbalimbali na visakramenti, Sala ya Kanisa na Ibada mbalimbali za Kanisa kama Ibada ya Neno la Mungu.

Kwa kuwa tumetumia mtazamo wa Kanisa wa mtume Paulo (Wakolosai 1, 18; Waefeso 1, 22-23) yaani Kanisa mwili wa Kristu (Kristu ni kichwa nasi tu viungo vingine vya mwili huo), nitalinganisha liturjia na damu katika mwili wa binadamu. Wazo nimelipata kutoka kwa Professor Paul Meyendorff. Fumbo la Pasaka ni kiini au mutima wa imani yetu. Moyo unaposukuma damu mwilini tunaweza kusikia mapigo ya moyo na kuona hata misuli ikitanuka na kusinyaa. Damu hii inazunguka mwili mzima hata sehemu ambayo hata tukioga huwa hatuizijali kwa sababu tunadhani hazina maana. Damu basi inasafirisha hewa safi na kutoa mwilini hewa chafu. Damu inasafirisha chakula na maji mwilini. Damu inasaidia mwili kutoa uchafu na sumu ndani yake. Damu inaupa uhai mwili wa mtu. Liturjia kama damu ndani ya mwili wa Kristu (Kanisa) inafanya kazi zinazofanana na hizo. Liturjia inatulisha Neno la Mungu. Liturjia inatulisha Mwili na Damu ya Kristu. Liturjia hasa ya Kitubio inatoa uchafu wote wa dhambi ndani ya mwili wa Kristu.  Liturjia inaujaza mwili wa Kristu neema takatifu na kuupatia nguvu za kuishi na kutenda kulingana na amri za Mungu katika maisha ya kila siku. Hapa tunaona uhusiano uliopo kati ya liturjia, imani na maisha ya kila siku. Katika Liturjia imani yetu inaongezeka na kuimarika na baada ya Ibada takatifu tunaishi yale tuliyoyaadhimisha. Matunda ya Ibada zetu yaonekane katika maisha yetu.

Kwa kifupi liturjia inaupa uhai Mwili wa Kristu yaani Kanisa. Bila liturjia Kanisa linakuwa halina uhai. Ndiyo maana Mtaguso wa pili wa Vatikano umesema kuwa Kanisa linaonekana hasa Askofu wa Jimbo anapoadhimisha Ekaristi Takatifu katika Kathedrale akiwa amezungukwa na mapadre, mashemasi na waumini wote wa Jimbo hilo wakisali Sala moja juu ya Altare moja (Sacrosanctum Concilium 41). Kwa hiyo nawaalika sana kushiriki mara nyingi Misa zinazoongozwa na Askofu wa Jimbo kila mara nafasi inapopatikana. Nadhani kwa leo imetosha juu ya mada hii ya liturjia. Nitaandika juu masomo ya liturjia kesho au kama sehemu ya pili ya mazungumzo yetu.

G. Mutarubukwa

Share this post
Repost0
To be informed of the latest articles, subscribe:
Comment on this post
G
ASANTE KWA MAFUNDISHO
Reply
G

Naomba uongelee pia kuhusu sehemu za Lituljia kwenye Ibada ya Misa Takatifu.

maana haya mafundisho yatasaidia wakati nikipata maswali niweze kujibu kwa kujiamini.
Asante.

Reply